Shinyanga, Tanzania - Shirika la Green Community Initiatives (GCI) kwa kushirikiana na Restless Development limefanikiwa kutoa mafunzo ya uraia na uongozi kwa vijana 50 kutoka kata mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa AU-EU Youth Voice Lab, unaolenga kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii, utawala na maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mwakilishi wa Restless Development kutoka YAWE, Bi. Cecilia Msangwa alisisitiza kuwa uongozi haupaswi kuhusishwa na nafasi rasmi za kisiasa au kiutawala peke yake.
"Kila kijana ana nafasi ya kuwa kiongozi katika jamii yake kwa kuanzisha mawazo mapya, kuhamasisha wengine na kushiriki kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi," alisema Bi. Cecilia.
Kupitia mafunzo hayo, vijana wamejifunza dhana ya uongozi, aina za uongozi, sifa za kiongozi bora, umuhimu wa uwajibikaji, utafiti wa taarifa sahihi, na mbinu za ushawishi kwa ajili ya kuleta mabadiliko chanya.
Bw. Peter Joseph kutoka YAWE/Restless Development aliwaelekeza vijana kuwa raia ana wajibu wa kufuatilia na kuelewa jinsi shughuli za maendeleo zinavyotekelezwa katika maeneo yao.
Akizungumza kwa niaba ya GCI, Bi. Maryciana William alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea vijana uelewa na uwezo wa kutumia maarifa waliyopewa katika kushiriki mijadala na shughuli za maendeleo ya jamii.
"Tunaamini vijana ndio injini ya mabadiliko. Tunapotambua umuhimu wao, tunajenga jamii yenye ushiriki, uwajibikaji na maendeleo endelevu," alisema.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Shinyanga, Bi. Salome Komba na Afisa Vijana, Bw. Enea Boniface wameipongeza GCI na Restless Development kwa hatua hiyo na kuwasisitiza vijana kutumia elimu waliyopata kwa vitendo - kwa kushiriki shughuli za kijamii na kutoa mawazo yatakayoboresha maisha ya wananchi.
Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo wakiwemo Emmanuel Robert, Mhoja Ibengwe, Eliya Bahame na Neema Songela wameahidi kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo kwa vijana wengine ili maarifa hayo yasiishie kwa washiriki 50 pekee, bali yafikie vijana wengi zaidi ndani ya Manispaa ya Shinyanga.
