Kuimarisha Mabaraza ya Watoto na Madawati ya Kijinsia: GCI Yazidi Kuwajengea Uwezo Watoto na Wanafunzi Shinyanga

Kuimarisha Mabaraza ya Watoto na Madawati ya Kijinsia: GCI yazidi kuwajengea uwezo watoto {Wanafunzi} katika kata za Itwangi Wilaya ya Shinyanga, Mkoani Shinyanga: Tarehe 07/05/2024.

Shirika la Green Community Initiatives limeendelea kutekeleza mradi wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mradi huu unalenga pia kuimarisha mabaraza ya watoto na madawati ya kijinsia katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Shinyanga. 

Leo shirika limefanya shughuli ya kuimarisha mabaraza ya watoto ikiwa ni moja ya hatua muhimu zinazochukuliwa chini ya mradi wa "Acha Ukatili", unaolenga kufanya kazi kwa bidii kuelekea kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miezi sita katika kata mbili za Itwangi na Nsalala wilaya ya Shinyanga, chini ya ufadhili wa Mfuko wa Ruzuku ya Wanawake Tanzania, Women Fund Tanzania Trust (WFT-T).

Kupitia mradi huu, GCI imekuwa ikiweka mkazo katika kutoa elimu ya kupinga mila na desturi kandamizi, elimu ya malezi bora, njia za kujilinda dhidi ya ukatili, na umuhimu wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili. Shughuli hii imekuwa ikilenga si tu kuwajengea uwezo watoto na wanafunzi katika kujitambua na kujilinda, bali pia kuwawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao.

Shughuli hii imekuwa na mafanikio makubwa katika kuwajengea uwezo watoto na wanafunzi, na kuwafanya wawe mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao. Walimu wa malezi katika Shule ya Msingi Luhumbo na Shule ya Msingi Zobogo wamepongeza juhudi za GCI na kuelezea umuhimu wa elimu hii katika kuboresha malezi na ulinzi kwa watoto.

"Tunashukuru sana Shirika la Green Community Initiatives kwa kuja na mradi huu. Watoto wetu sasa wanafahamu haki zao na wanajua jinsi ya kujilinda dhidi ya ukatili. Tunaona mabadiliko makubwa katika tabia zao na hata uwezo wao wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili umekuwa wa juu sana." - Mwalimu wa Malezi, Shule ya Msingi Zobogo.

Watoto nao wameonyesha furaha na hamasa katika kupokea elimu hii, wakiitambua kama chachu ya mabadiliko katika maisha yao na jamii kwa ujumla.

"Tunajifunza mambo mengi mazuri kuhusu haki zetu na tunajua sasa tunapaswa kujilinda. Tunashukuru Shirika la GCI kwa kutuletea mradi huu na tunajivunia kuwa sehemu ya mabaraza ya watoto yanayosaidia kuleta mabadiliko katika jamii yetu." - Mtoto mwanafunzi, Shule ya Msingi Luhumbo.

Kupitia jitihada hizi za kuwajengea uwezo watoto na wanafunzi, GCI inaendelea kuonyesha dhamira yake ya kuleta mabadiliko chanya na kuimarisha ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili. Tunachukua fursa hii kuwashukuru wadau wote waliochangia kufanikisha mradi huu na kuwaomba waendelee kutuunga mkono katika safari yetu ya kuwaletea watoto na jamii kwa ujumla maendeleo endelevu na ustawi.