Recent Posts

KIKAO CHA ROBO MWAKA KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA KUPINGA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO NDANI YA HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA

Shirika la Green Community Initiativeives limeweza kushiriki kwenye kikao cha Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Kikao  cha Robo Mwaka katika utekelezaji wa MTAKUWWA) kama wadau watekelezaji wa Miradi ya kupinga Ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kikao hicho kimefanyika leo Machi 20, 2023 katika Makao Makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yaliyopo Kata ya Iselamagazi, na kuwasilishwa taarifa za utekelezaji wa mradi wa kupinga matukio ya ukatili kutoka mashirika mbalimbali, ambayo yalikuwa yakitekeleza mradi huo wilayani Shinyanga kwa kipindi cha miezi mitatu, kwa ufadhili wa Mfuko wa Ruzuku wa Wanawake Tanzania (WFT-Trust).

Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wilayani Shinyanga Joram Magana, akizungumza kwenye kikao hicho amesema Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yamekuwa na mchango mkubwa kupunguza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wilayani Shinyanga.

Amesema Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa sasa matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto yamepungua kwa kiasi kikubwa, ambapo jamii imekuwa na uelewa mkubwa wa madhara ya kufanya ukatili, kutokana na elimu kutolewa ipasavyo kwa wananchi. 

Vile vile naye Mratibu wa Mpango kazi wa kudhibiti na kuzuia ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) wilayani Shinyanga Bi. Aisha Omary, amesema miradi mbalimbali iliyofanywa na wadau kwa umoja kama Shinyanga EVAWC kuelimisha jamii juu ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto imeleta matokeo makubwa Sana ambako viongozi wa Mila pamoja na SUNGUSUNGU wameitikia mafunzo hayo nakuonesha mabadiliko makubwa ikiwemo kuanza kuchukulia hatua matukio yanayoendana na ukatili ndani ya jamii ya watu wa Shinyanga kwa wale ambao wanafanya ukatili.

“Tunaushukuru Mfuko wa Ruzuku wa Wanawake Tanzania (WFT-Trust) kwa kufadhili na kutekelezwa mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto hapa wilayani Shinyanga ambao umesaidia kupunguza ukatili wa wanawake na watoto,”amesema Aisha.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi Ofisa Oparesheni kutoka Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Emmanuel Galiyamoshi akimwakilisha Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo Janeth Magomi, amewapongeza wadau wa maendeleo kwa kufanya kazi kubwa ya kupinga matukio ya ukatili, na kuahidi Jeshi litaendelea kushirikiana nao ili kukomesha matukio hayo.

Aidha, ametaja baadhi ya Changamoto ambazo wanakabiliana nazo ikiwamo ufinyu wa chumba katika vituo vya Polisi, kwa ajili ya kuhifadhi Madhura ambao wanafanyiwa vitendo vya ukatili na kusababisha kuharibika kwa Ushahidi, sababu binti akirudi kwao anarubuniwa na wazazi na kumkana mtuhumiwa ambaye alimtaja awali kuwa kampatia ujauzito.

Nayo Mashirika ambayo yaliwasilisha taarifa zao za utekelezaji wa Mradi wa kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia wilayani Shinyanga kwenye kikao hicho cha Robo mwaka wakiwemo GCI, YAWE, TAI, WAEDO, SHY PRESS, YAWL, Rafiki SDO pamoja na Radio Faraja, wametaja mafanikio kwamba jamii imekuwa na uwelewa mkubwa wa kupinga ukatili, na wamekuwa wakitoa taarifa za viashiria vya ukatili pamoja na watu ambao wameshafanyiwa ukatili wakiendelea kutoa taarifa.