Green Community Initiatives (GCI) yatambulisha rasmi Mradi mpya "My Healthy Project" katika mkutano wa WDC kata ya Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga!
1. Kuhusu Mradi
Mradi wa “Afya Yangu” unalenga kuimarisha elimu ya hedhi salama na kujenga vyumba maalum kwa ajili ya usafi wa hedhi (Menstrual Hygiene Room) kwa wasichana walioko katika Shule ya Sekondari Imenya iliyopo Kata ya Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Mradi huu unalenga kutatua changamoto ya wanafunzi wa kike kukosa mazingira salama na stahiki wakati wa kipindi cha hedhi, hali inayochangia utoro na kushuka kwa ufaulu wa kitaaluma. Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 25 ya wasichana hupoteza siku 3 hadi 5 za masomo kila mwezi kutokana na ukosefu wa mazingira bora ya usafi wa hedhi (UNICEF, 2021).
Mradi huu unalenga kuboresha mazingira ya afya, heshima na ujumuishaji wa wasichana shuleni kwa kuwawezesha kupata huduma za usafi, faragha, maji, na elimu ya afya ya uzazi. Mradi huu unalingana na sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Mpango wa Taifa wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto (One Plan II) pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika maendeleo.
2. Lengo Kuu na Malengo Mahususi
Lengo Kuu: Kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kike kupitia ujenzi wa vyumba maalum vya usafi wa hedhi katika Shule ya Sekondari Imenya.
Malengo Mahususi:
- Kujenga vyumba viwili vya usafi wa hedhi chenye vifaa muhimu kama vyoo, maji, sabuni, pedi na ndoo za kutunzia taka.
- Kutoa elimu kwa wanafunzi juu ya hedhi salama, afya, usafi wa hedhi na heshima ya mwili.
- Kupunguza utoro wa wanafunzi wa kike shuleni unaosababishwa na changamoto za hedhi kwa asilimia 30 ndani ya miezi 6.
3. Eneo la Utekelezaji
- Mradi utafanyika katika Shule ya Sekondari Imenya, Kata ya Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mkoa wa Shinyanga – Tanzania.
4. Shughuli za Mradi
- Kutoa elimu ya afya na hedhi salama kwa wanafunzi vijana wa kike na wa kiume.
- Kuanzisha na kuimarisha klabu za afya katika Shule za Msingi na Sekondari Imenya kwa ajili ya uendelevu wa elimu ya afya shuleni.
- Kujenga vyumba vya kujisitiri (Menstrual Hygiene Rooms) katika Shule ya Sekondari Imenya ili kuwezesha mabinti kujistili kwa usalama na heshima wanapokuwa shuleni.
