Recent Posts

GCI YAHIMIZA JAMII MKOANI SHINYANGA KUPIGA VITA MILA NA DESTURI KANDAMIZI ZINAZOCHOCHEA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO

GCI YAHIMIZA JAMII MKOANI SHINYANGA KUPIGA VITA MILA NA DESTURI KANDAMIZI ZINAZOCHOCHEA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO

Meneja Mradi wa Shirika la Green Community Initiatives (GCI) Bwana Ngolelwa Enos Masanja amewaomba wazazi na walezi katika jamii kuwa  mabalozi wa kupiga vita mila na desturi kandamizi zinazochochea ukatili kwa wanawake na watoto.

Bwana Ngolelwa amebainisha hayo wakati akitoa semina ya kupinga ukatili katika uwanja wa shule ya msingi Lohumbo iliyopo kata ya Itwangi na kuwaomba wananchi wote kuwa mabalozi wa kupinga ukatili kuanzia ngazi ya familia kwa kuibua na kuripoti changamoto mbalimbali zinazochochea ukatili.

‘‘…hapa kata ya Itwangi tumepokea kesi nyingi sana za ukatili wa kiuchumi wanaume wenzangu tunatumia rasilimali za familia ikiwemo mazao,fedha na mali zingine kwa mambo yasiyo ya msingi ikiwemo kuhonga hayo yote hayana faida ndani ya familia zetu tuache, pia tumepokea kesi za wazazi na walezi kuwazuia watoto kwenda shule wengine wanawaruhusu lakini wakirudi kutoka shuleni hawawapi chakula huo pia ni ukatili niwaombe tunapoona viashiria vya ukatili tusiogope kuyaibua maovu na kuyafikisha kwa viongozi wetu wa serikali ili kupinga ukatili katika familia na jamii yote’’

Kwa upande wao viongozi wa serikali kata ya Itwangi wameahidi kuendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali yanayojitokeza kutoa elimu ya kupinga ukatili  ikiwemo shirkika la Green Community Initiatives (GCI) na kuwaomba wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi  inapotokea fursa ya kupata elimu hiyo.

‘‘… wazazi na walezi wenzangu niwaombe tuwajibikie vema jukumu la malezi na makuzi kwa watoto wetu tuwapende, tuwajari, tuwasikilize na kuwalinda na mambo yote ya ukatili yaliyomo katika familia na hata jamii zetu pia tutambue umuhimu wa elimu jamoni tuwapeleke watoto shuleni huko watafundishwa mabaya ya ukatili na namna ya kuyafikisha kwetu na tutawasaidia kutimimiza ndoto zao’’ Amesema kaimu Afisa maendeleo ya jamii kata ya Itwangi Bi. Fatuma Mremi

Kamuli Sanyiwa Makomango ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Itwangi amewasisitiza wananchi kuitumia vema elimu waliyoipata kwani elimu haina mwisho na inaendelea kuishi.

‘‘ndugu zangu tusichoke kujifunza kila siku kwani elimu haina mwisho na inaendelea kuishi kila kukicha leo GCI wamefika hapa wametupa elimu ya kupinga ukatili niwaombe elimu hii tukaitumie katika familia zetu mpka ngazi ya jamii na sisi viongozi wenu tuwahakikishie kuendelea kushirikiana na haya mashirika kuja kutoa elimu’’

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika semina hiyo wamelipongeza shirika la Green Community Initiatives (GCI) kwa elimu waliyoitoa na kuahidi kwenda kuifanyia kazi elimu hiyo na kuwa mabalozi wa kupinga ukatili katika familia jamii na kuliomba shirika hilo kuendelea kutoa elimu ili kutokomeza ukatili. 

Sanjari na hayo timu ya Majimaji FC imefanikiwa kushinda goli 4 – 0 Mzalendo FC katika mchezo wa ufunguzi wa semina hiyo na kutwaa kombe.